KWAHERI DADANGU CHANYA

KWAHERI DADANGU CHANYA
(Last Updated On: January 22, 2018)

Naanza kwa jina lake, mtukufu maulana
Atupe rehema zake, atuongoze bayana
Kila mtu ana yake, sikuye hawezi kana
Kwaheri dadangu Chanya, pema mola akulaze

Umeyatenda ni mengi, Agnesi hadi Loreto
Chuoni pia kwa wingi, bila laiti majuto
‘Katupa furaha nyingi, yenye sifa ya uzito
Kwaheri dadangu Chanya, pema mola akulaze

Tabasamu yako tamu, kila mara hadi sasa
Kicheko ja kilaamu, chenye sifa ya kisasa
Maneno tamu hamamu, hekima bila siasa
Kwaheri dadangu Chanya, pema mola akulaze

Twakukumbukia wema, ulotenda ni kathiri
Na mengi uliyosema, hatuwachi kukariri
Mola akulaze pema, peponi akusitiri
Kwaheri dadangu Chanya, pema mola akulaze

Mswiba umetuswibu, umetuacha swahibu
Tulimpenda ajabu, halingani na dhahabu
Hatuna katu majibu, kwa kifo kilikuswibu
Kwaheri dadangu Chanya, pema mola akulaze

Ni pigo kwetu chuoni, hata chuoni Loreto
‘Metuacha huzuni, na maisha ya majuto
Tulikuenzi mwandani, kipenzi chetu cha uto
Kwaheri dadangu Chanya, pema mola akulaze

Rambirambi nyingi sana, ziwafikie nyumbani
Farajaze maulana, kwa ndugu na majirani
Inshallah tutamwona, kipenzi chetu peponi
Kwaheri dadangu Chanya, pema mola akulaze

Rabana yetu sikia, waja tunakulilia
Sisi kwako tunajua, ni lazima kurejea
Tuelekeze hatua, tusije potea njia
Kwaheri dadangu Chanya, pema mola akulaze

©Silah Moh’d
All rights reserved
©2017

share

Recommended Posts

April 02, 2021